Pasipo Roho Hakuna Uhai

2026-05-24
Dominika ya Pentekoste
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Mdo 2:1-11

Somo la Pili: 1 Kor 12:3-7, 12-13

Injili: Yn 20:19-23

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Ndugu wapendwa leo tunaadhimisha sherehe ya Pentekoste ambayo ni siku 50 baada ya Pentekoste. Ni utimilifu wa Fumbo la Pasaka. Fumbo la Pasaka linatimilizika kwa kuzaliwa kwa Kanisa. Kwamba Kristo anaendelea kuwepo katika kanisa lake kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ishara kubwa ya uwepo wa Roho Mtakatifu katika kanisa ni umoja. Hivyo Roho Mtakatifu ni upendo unaotuleta pamoja kama viungo vya Kristo.

Homilia

Pentekoste kwa Wayahudi ilikuwa ni kumbukumbu ya agano la Sinai, ni Kumbukumbu ya kupokea amri kumi za Mungu (Law 23:15-22). Pia ni sikukuu ya Mavuno. Kwa wakristo Pentekoste ni utimilifu wa fumbo la Pasaka, ni kushukiwa Roho Mtakatifu kwa mitume, yaani kwa kanisa, ni kuzaliwa kwa kanisa. Na hivyo ni ushindi dhidi ya hofu, dhambi, utengano, majivuno, kiburi, kinachotokana na utengano na uwepo wa Mungu katika maisha yetu.

Somo la I: Katika somo la kwanza tunasikia habari za Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume siku ya Pentekoste. Kulikuwako na watu mbalimbali waliosafiri kwa sikukuu ya Pentekoste. Mitume baada ya kumpokea Roho waliwahubiria watu kila mtu kwa lugha yake. Walipokea uwezo wa kunena kwa lugha mbalimbali. Roho aliwapa uhai watu wote waliokuwako huko.

     Tofauti na wakati wa mnara wa Babeli, Roho anawaleta Pamoja. Anawaunganisha, walishinda majivuno, maangamizi, Roho analeta mwanzo mpya wa kanisa. Roho anawafanya kuwa hai tena. Roho analiunda kanisa toka katika lugha, kabila, taifa, rangi, na karama mbalimbali. Sote tunaunganishwa na upendo wa Mungu kwa njia ya rangi yake. Hivyo kama Wakristo tunapaswa kuongea lugha moja tu ya upendo sio lazima yawe maneno bali mioyo yetu ijazwe Roho wa Mungu na tuzungumze lugha moja ya Upendo.

Somo la II: Katika somo la pili tunaonyeshwa kwamba Roho Mtakatifu ndiye mgawaji wa karama zote. Karama katika maisha yetu ni tofauti na nyingi. Ila mgawaji ni mmoja tu Roho Mtakatifu. Pana tofauti ya karama na huduma bali Roho ni yeye yule. Cha msingi, vipaji, karama, huduma na ujuzi vyote vimtangaze Kristo. Maana vyote ni vyake.

     Katika safari yetu ya maisha kama wakristo, tunapaswa kutumia karama, vipaji, uwezo na offisi zetu kuwashirikisha na kuwasaidia wenzetu. Tatizo limwkuwa kwamba tumekuwa tukitumia karama zetu kuwachapia wenzetu, vyeo vyetu kuwachapia wenzetu, uwezo wetu kuwanyanyasa wenzetu, kuwadalilisha wenzetu, kuwanyanyasa wadogo na maskini. Tutumie vipaji na vipawa vyetu kwa kumtumikia Mungu na jirani. Na huo ndio uhai na utajiri wa Kanisa.

Injili: Katika somo la Injili tunaona Yesu anawatokea wanafunzi wake wana hofu ya Wayahudi wamejifungia ndani. Yesu anawaondoa hofu na kuwatakia amani na kuwavuvia Roho Mtakatifu. Hii ndio ishara ya kuzaliwa tena upya. Pumzi aliypuliziwa Adamu akawa hai, Pumzi hiyo Yesu anawapulizia Mitume, yaani kanisa na linakuwa hai tena. Uhai unarudishwa kupitia Roho Mtakatifu, Hofu inaondoka amani inatawala na mamlaka juu ya dhambi yanadhihirishwa.

     Ukimpokea Roho Mtakatifu unakuwa hai tena na kuwa na mamlaka dhidi ya dhambi na shetani. Unashinda kiburi, unashinda majivuno, unashinda hofu, unashinda utengano, unashinda ugomvi, unashinda dhuluma, unashinda unyanyasaji. Leo ni siku ya muhumu sana katika kanisa ukristo wetu maana tunaalikwa kuwa hai tena. Kushinda utengano. Kuwa kitu kimoja kama vioungo vya Kristo.

     Tumwombe Roho Mtakatifu aendelee kututakasa sisi na kulitakasa kanisa lake kwa kulijalia umoja, amani, upendo na mshikamano. Mungu anayekamilisha fumbo la Pasaka kwa ujio wa Roho Mtakatifu anajifunua kwetu kwa njia ya Utatu Mtakatifu. Tumwombe Mungu kupitia karama zetu tuweze kumjua yeye kupitia Roho Mtakatifu kwa kuyaishi Matunda yake.